- Author, Tom Brada
- Nafasi, BBC
Onyo: Makala hii ina maudhui ya kusikitisha
Miguu ya Elaine Foo ina makovu makubwa - kila kovu ni ukumbusho wa operesheni ya kurefusha miguu ambayo ilikwenda vibaya.
Tangu 2016, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 49 amefanyiwa upasuaji mara tano na kumaliza akiba yake ya pesa. Amemchukulia hatua za kisheria daktari wake wa upasuaji, kesi hiyo iliisha mwezi Julai, kwa daktari huyo kukubali kumlipa fidia lakini kakataa kukiri kufanya kosa lolote.
Wakati fulani, Elaine alikuwa na msumari wa chuma katikati ya mfupa na wakati mwingine, anasema miguu yake alihisi kama inaungua kutokea ndani.
Daktari wake amekanusha kufanya uzembe wowote na anasema baadhi ya matatizo yalitokana na mambo ambayo Elaine alikuwa ameonywa, na mengine yalitokana na matendo yake mwenyewe.
Lishe bora kwa watu wembamba wanaotaka kuongeza miili
Je, unalijua taifa lenye watu warefu zaidi duniani?
Upasuaji hatari wa kubadili maumbile ambao wanaume wanafanyiwa zaidi na zaidi
Elaine alichukia kimo chake
"Nikiwa na miaka 12, nilikuwa mrefu kuliko wasichana wengi. Kufikia miaka 14, nilikuwa mfupi ghafla kuliko kila mtu. Nilihisi watu warefu walikuwa na fursa nyingi zaidi."
Elaine anaamini alikuwa na tatizo la kisaikolojia la kuchukia maumbile yake. Ni hali ambayo mtu huona kasoro katika mwonekano wake bila kujali jinsi wengine wanavyomuona. Athari ya hali hiyo inaweza kuwa mbaya.
Akiwa na umri wa miaka 25, Elaine alikutana na makala kuhusu kliniki ya China ambapo watu walikuwa wakifanyiwa upasuaji ili kufanya mifupa yao ya miguu kuwa mirefu. Makala hiyo ilionekana kuwa na maelezo ya kutisha, lakini ilimfanya Elaine kuvutiwa.
Miaka kumi na sita baadaye, Elaine aligundua kliniki ya kibinafsi inayotoa matibabu hayo huko London. Ilikuwa ikitolewa na daktari wa upasuaji wa mifupa Jean-Marc Guichet, mtaalamu wa kuongeza viungo ambaye alikuwa ameunda kifaa chake cha kurefusha - Guichet Nail.
"Ulikuwa wakati wa haleluya, kwa sababu ningeweza kufanya operesheni London na ningeweza kupona nyumbani," anakumbuka.
"Daktari Guichet alikuwa muwazi kuhusu mambo ambayo yanaweza kwenda vibaya. Majeraha ya neva, kuganda kwa damu, uwezekano wa mifupa kutoungana tena.
"Lakini nilifanya utafiti wangu, na nilikwenda kwa daktari wa gharama kubwa na nilitarajia huduma ya matibabu iwe bora. Ndoto yangu ilikuwa kukua kutoka futi 5 nchi 2 (1.57m) hadi futi 5 nchi 5 (1.65m)."
Tarehe 25 Julai, kwa gharama ya karibu pauni za Uingereza 50,000, aliingia katika upasuaji na kuanza mchakato ambao ungebadilisha maisha yake.
Taratibu za kurefusha miguu zinapatikana katika kliniki za kibinafsi duniani. Inaweza kugharimu kutoka pauni 15,000 au zaidi ya 150,000.
Baada ya kuamka alifurahi sana, kwa sababu ilionekana kama hakuna kilichotokea. Hakuna maumivu. Lakini dakika 90 baadaye, maumivu yalianza.
Alikuwa akihisi kama mtu alikuwa akiipika miguu yake. Kama kuchomwa kutoka ndani. "Usiku ule wa kwanza nilipiga kelele hadi saa kumi na mbili asubuhi, hadi nililala nikipiga kelele.”
Kwa operesheni hii, maumivu fulani yanatarajiwa. Ni operesheni ambayo mifupa ya mguu imevunjwa mara mbili na fimbo ya chuma imewekwa ndani.
Fimbo za chuma huongezwa urefu hatua kwa hatua ili kuongeza urefu wa mguu na kutengenisha nusu mbili za mfupa. Mifupa iliyokatwa hupona hatua kwa hatua, ili kujaza pengo la kati.
"Mchakato wa kurefusha huchukua muda wa miezi miwili au mitatu na kisha kuna muda mara mbili ya huo kabla ya kupona sawa sawa," anasema Prof Hamish Simpson, mjumbe wa zamani wa baraza la Mifupa la Uingereza. "Kwa watu wengi, itachukua kama mwaka."
Matatizo yalipoanza
Mara tu upasuaji ulipokwisha, mchakato wa kurefusha mguu wa Elaine ulianza. Lakini wiki mbili baadae, ndipo mambo yalipoanza kuharibika.
"Nilikuwa nikisikia maumivu kwenye mguu wangu wa kushoto. Kisha usiku mmoja, nilipokuwa nikizunguka-zunguka kitandani, nilisikia sauti kama ya kit kat, ikifuatwa na maumivu makali.”
Elaine alikwenda kufanyiwa uchunguzi, ambao ulithibitisha hofu yake. Msumari wa mguu wake wa kushoto ulikuwa umekatika kwenye fupa la paja. Alifadhaika, lakini anasema aliambiwa asiwe na wasiwasi na Dk Guichet.
"Aliniambia kuwa unachohitaji kufanya sasa sio kuwa na wasiwasi. Subiri nipone, na nikishapona tutaanza tena mchakato huo.”
Waliendelea kurefusha mguu wa kulia wa Elaine, huku wakipanga operesheni nyingine ya mguu wake wa kushoto - ambao hatimaye ungerefushwa kwa kiasi sawa na wa kulia.
Elaine anasema aliambiwa operesheni ya ziada ingegharimu maelfu ya pauni, lakini hakuwa na tatizo kulipa kama ingemaanisha angeweza kukamilisha mchakato huo.
Kufikia Septemba, mguu wake wa kulia ulikuwa umefikia lengo lake la sentimita 7. Lakini mfupa wa mguu wa kushoto wa Elaine ulionyesha ukosefu wa ukuaji. Na tofauti kati ya mguu wake wa kulia na wa kushoto ilikuwa ikisababisha matatizo, na kupindisha uti wa mgongo na kumwacha katika maumivu ya mara kwa mara.
Elaine alimgeukia Dk Guichet kwa usaidizi, ambaye alipanga upasuaji mwingine katika kliniki huko Milan. Aprili 2017, walianza tena mchakato wa kurefusha mguu wa kushoto wa Elaine huku wakiweka uboho kusaidia mfupa wa mguu wa kulia kukua. Baada ya upasuaji, Elaine aliamka na kupata habari mbaya zaidi.
"Daktari Guichet aliniambia msumari ulikuwa umekatika alipokuwa akiutoa."
Siku tatu baadaye, akiwa hana uwezo wa kutembea, akiwa amekata tamaa nyumbani, Elaine alirudi London. Anasema mawasiliano na Dk Guichet yaliharibika na kufikia majira ya joto uhusiano wa daktari na mgonjwa ulikuwa umevunjika.
Hakujua mahali pengine pa kuelekea na kufikia Julai 2017 alifanikiwa kuonana na daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa London.
Anasema mtaalamu huyo alimwambia "hii haitakuwa safari fupi."
"Ilinibidi nijitayarishe kwa angalau miaka mitano ya matibabu kabla ya kupona kikamilifu," anasema.
Miaka minane baada ya upasuaji wa awali Elaine anasema bado anapata nafuu kutokana na majeraha yake ya kiakili na kimwili.
"Kuanzia 2017 hadi 2020 nilijificha kutoka kwa ulimwengu. Nilikuwa peke yangu, sina kazi, sina senti na mlemavu.”
Vita vya Kisheria
Vita vya kisheria vilivyodumu kwa miaka minne hatimaye vilisuluhishwa Julai wakati Dk Guichet alipokubali kumlipa Elaine kiasi kikubwa cha pesa ili kumaliza madai dhidi yake – lakini hakukubali makosa.
Wakili wa daktari huyo wa upasuaji alikanusha uzembe wowote wa Dk Guichet, akiiambia mahakama: "Kesi ya Dk Guichet ni kwamba hakukuwa na uzembe, kuvunjika na kuchelewa kwa mfupa kupona ni matatizo ya bahati mbaya yasiyo ya uzembe ambayo Bi Foo alionywa kabla ya upasuaji. Na ukuaji mdogo wa mfupa wa upande wa kulia ulichochewa na Bi Foo kutumia dawa za kupunguza mfadhaiko bila kujulikana na kwa kuongeza kwa makusudi urefu wa msumari kwenye mguu wake wa kulia zaidi ya urefu uliokubaliwa.”
Pia alidai mahakamani kwamba Bi Foo, alikataa mara kwa mara kufuata ushauri wa Guichet na alipuuza tiba ya mwili.
Elaine anapinga madai haya yote. Anasema dawa za kupunguza msongo wa mawazo hazina uhusiano na matatizo hayo na anamlaumu daktari kwa kile kilichompata.
Elaine alidhani alikuwa salama kwa sababu alikuwa akilipa pesa nyingi. Lakini amelipa zaidi ya fedha.
"Nilipoteza miaka ya maisha yangu. Mtu akiniuliza leo ungefanya operesheni, kama ungejua utapitia haya yote? Nitasema, 'Hapana, asante sana'."
Lishe bora kwa watu wembamba wanaotaka kuongeza miili
Je, unalijua taifa lenye watu warefu zaidi duniani?
Upasuaji hatari wa kubadili maumbile ambao wanaume wanafanyiwa zaidi na zaidi
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah
Imehaririwa na Maryam Abdalla